Jumamosi 31 Oktoba 2026 - 15:10
Kuwepo makabila mbalimbali ya Iran na ushiriki wa Shia na Sunni katika shughuli za kijamii ni dhihirisho la mshikamano wa kitaifa na kidini

Hawza/ Mamusta Iqbal Bahmani, mwakilishi wa wananchi wa Kurdistan Iran, katika Baraza la Wataalamu wa Uongozi, huku akifafanua dhana ya Qur’ani ya Ba‘thah (kupewa utume na kuanzisha mwamko), ameitaja kuwa ni harakati ya kumkomboa mwanadamu kutokana na dhuluma na udikteta, na kufanikisha tunu za Mwenyezi Mungu. Pia ameeleza kuwa mwamko ya wananchi wa Iran ni msingi wa kuibuka mwamko wa Kiislamu na kuimarika umoja wa Umma wa Mtume Mtukufu (saww).

Kwa mujibu wa taarifa ya Idara ya Kimataifa ya Shirika la Habari la Hawza,  Mamusta Iqbal Bahmani, mwakilishi wa wananchi wa Mkoa wa Kurdistan katika Baraza la Wataalamu wa Uongozi, katika kikao cha saba cha kimataifa cha “Mwamko Mpya wa Umma wa Muhammad (saww)”, kilichofanyika Jumatano, kwa juhudi za Jumuiya ya Kimataifa ya Qadimun, alifafanua dhana ya Qur’ani ya Ba‘thah, na kuitaja kuwa ni harakati ya kumkomboa mwanadamu kutokana na dhuluma na udikteta, kufanikisha tunu za Mwenyezi Mungu na kurejea katika umoja na udugu wa Kiislamu.

Akirejelea aya ya pili ya Suratul-Jumu‘ah:

هُوَ الَّذِي بَعَثَ فِي الْأُمِّيِّينَ رَسُولًا مِنْهُمْ يَتْلُو عَلَيْهِمْ آيَاتِهِ وَيُزَكِّيهِمْ وَيُعَلِّمُهُمُ الْكِتَابَ وَالْحِكْمَةَ

“Yeye ndiye aliyemleta Mtume miongoni mwa watu wasiojua kusoma na kuandika, kutoka miongoni mwao wenyewe, awasomee aya Zake, awatakase na kuwafundisha Kitabu na Hikima.”

Alisema: Katika Qur’ani Tukufu, dhana ya Ba‘thah ina maana pana zaidi kuliko mwamko wa muda mfupi. Inamaanisha kuamsha, kuanzisha mwendo na kumtuma mtu kwa ajili ya kutekeleza jukumu maalumu. Vilevile, kupewa utume Mitume wa Mwenyezi Mungu kulifanyika kwa lengo la kuwaongoza wanadamu kutoka katika giza la dhambi, dhuluma na utawala wa matwa'ghuti kuelekea kwenye nuru ya Mwenyezi Mungu na saada ya dunia na Akhera.

Bahmani aliongeza: Umma ulioamshwa unapaswa kufuata ujumbe uleule walioubeba Mitume, yaani kufundisha Kitabu na Hikima, kuwatakasa wanadamu na kuirekebisha jamii. Akirejelea mwenendo wa Mitume na mawalii wa Mwenyezi Mungu, akiwemo Hasan al-Basri, Sheikh Abdul-Qadir Jilani na Bahauddin Naqshbandi, alisisitiza umuhimu wa kuzitakasa nafsi za wanadamu na kujikomboa kutoka katika utawala wa matwa'ghuti.

Mwakilishi wa wananchi wa Kurdistan katika Baraza la Wataalamu wa Uongozi, alielezea pia kukamilisha fadhila za kimaadili kuwa ni miongoni mwa malengo ya kupewa utume Mtume wa Uislamu (saww), na kurejelea hadithi isemayo:

إِنَّمَا بُعِثْتُ لِأُتَمِّمَ مَكَارِمَ الْأَخْلَاقِ

“Hakika nimetumwa ili nikamilishe maadili mema.”

Kwa mujibu wa maelezo yake, kupewa utume Mitume, kunasimama dhidi ya tunu za Kijahiliya, misimamo ya kibaguzi ya kikabila, dhuluma na udikteta. Lengo lake ni kuinua kiwango cha maadili na kurekebisha maisha ya mwanadamu, katika ngazi ya mtu binafsi na jamii.

Akizungumzia dhana ya mwamko wa wananchi wa Iran, alisema: Mwamko wa taifa la Iran unaweza kuchukuliwa kuwa ni harakati ya kiutambuzi na mabadiliko makubwa katika mfumo wa fikra na tunu, ambayo kwa mujibu wa maelezo yake, umevuta hisia za watu duniani kuhusu suala la udikteta, ubeberu na tamaa ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa kuwatawala wengine.

Bahmani, akisisitiza nafasi ya umoja wa makabila na madhehebu katika mwenendo huu, aliongeza: Kuwepo makabila mbalimbali nchini Iran, kuanzia Wakurdi na Waturuki hadi Waajemi, Waarabu na Wabaluchi, pamoja na ushiriki wa Shia na Sunni katika shughuli za kijamii, ni dhihirisho la mshikamano wa kitaifa na kidini.

Akirejelea aya isemayo:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ

“Hakika waumini ni ndugu.”

Pamoja na amri ya Qur’ani isemayo:

وَاعْتَصِمُوا بِحَبْلِ اللَّهِ جَمِيعًا وَلَا تَفَرَّقُوا

“Na shikamaneni kwa kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane.”

Alieleza kuwa; umoja na udugu ni miongoni mwa matunda muhimu zaidi yanayotarajiwa kupatikana kutokana na mwamko wa Umma wa Kiislamu.

Aidha, alizungumzia kuonekana alama za Muqawama na bendera za Iran na Palestina katika mikusanyiko ya wanafunzi wa vyuo vikuu barani Ulaya na Marekani. Alilitaja jambo hilo kuwa ni ishara ya kuongezeka uelekezaji wa hisia katika suala la Palestina na athari za maendeleo yanayotokea Iran katika maoni ya umma.

Mamusta Bahmani aliendelea kwa kutaja mbinu tatu za vitisho, kutoa vishawishi na kuzusha hofu kupitia mitandao ya vyombo vya habari, kuwa ni miongoni mwa nyenzo ambazo, kwa mujibu wa mtazamo wake, madola yenye misimamo ya kutawala wengine huzitumia ili kuyaathiri mataifa. Alisisitiza umuhimu wa kuwa macho, kuwa na ufahamu na kudumisha ushiriki wenye uwajibikaji wa wananchi mbele ya mashinikizo hayo.

Vilevile, akirejelea hadithi isemayo:

إِنَّ اللَّهَ يَبْعَثُ لِهَذِهِ الْأُمَّةِ عَلَى رَأْسِ كُلِّ مِائَةِ سَنَةٍ مَنْ يُجَدِّدُ لَهَا دِينَهَا

“Hakika Mwenyezi Mungu humleta kwa ajili ya Umma huu, mwanzoni mwa kila karne, mtu ambaye huufanyia upya dini yake.”

Alisisitiza umuhimu wa kuhuisha dini kwa kuendelea na kurekebisha upotovu wa fikra na kijamii. Pia, akikumbusha tofauti iliyowekwa baina ya Uislamu halisi wa Muhammad na Uislamu wa Kimarekani katika fikra za Imam Khomeini (ra), alisema: Uislamu wa kweli una uhusiano wa karibu na tunu za Mtume wa Uislamu (saww), kupambana na udikteta na ubeberu, pamoja na kutetea heshima na utu wa wanadamu.

Mwisho, alieleza matumaini yake kwamba Waislamu, kwa kufuata mwenendo wa Mtume Mtukufu (saww), Ahlul-Bayt (as), Mawalii wa Mwenyezi Mungu na Makhalifa Waongofu, watapiga hatua katika njia ya kufufua tunu za Kiislamu, kuimarisha umoja na kukabiliana na dhuluma na udikteta.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha